Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima,amesema kuna haja ya siku ya Wanaume Duniani inayoadhimishwa kila Novemba 19 kutambuliwa rasmi nchini kama inavyoadhimishwa siku ya Wanawake, ili waweze kutambua nafasi yao katika kulinda, kuendeleza familia na kupinga ukatili.
Akizungumza katika kongamano maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani kwa kanda ya ziwa lililofanyika wilayani Bukombe Mkoani Geita, Dkt. Gwajima amesema kuitambua siku hiyo rasmi, kutatoa nafasi kwa Wanaume kushiriki kikamilifu katika mijadala kuhusu haki za kijinsia, malezi bora na ustawi wa familia.

Amesema, “hatuwezi kuendelea mbele kama wanaume hawajaelewa dhana ya usawawa kijinsia kwakuwa wao ni wababa ni muhimu waongee na watoto wao wa kike na wakiume kuhusu masuala haya. Sera mpya ya maendeleo jinsia na wanawake ya mwaka 2023, wanaume wameingizwa baada ya kubaini wanawake hawawezi kuendelea mbele kama wanaume watakuwa hawajaielewa dhana hiyo na kwenda kuzungumza na wanawake.”
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, kutambuliwa kwa siku hiyo pia kutapunguza ukatili wa kijinsia kwakuwa wanaume watakuwa sehemu ya Suluhisho kwa kushiriki majadiliano na kampeni zinazolenga kumaliza ukatili dhidi ya wanawake,watoto na makundi mengine.