Wakala wa Usajili wa Leseni na biashara nchini Tanzania ( BRELA) Umewafutia usajili makampuni 11 ya hapa nchini Tanzania kuanzia tarehe 27 Februari kwa mujibu wa kifungu cha sharia No 400A cha Sheria ya makampuni sura 212

Akiongea na wanahabari ofisini kwake leo jijini Dar es salaam, Afisa mtendaji mkuu wa BRELA, Julias Nyaisa amesema sababu za kufutwa kwa kampuni hizo ni kukiukwa kwa masharti ya kifungu cha 400A (1)
(e) cha sharia tajwa hapo juu kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika katiba za kampuni hizo na miongozo ya uendeshaji wa kampuni wakati wa usajili.

Nyaisa amezitaja kampuni zilizofutiwa usajili ni pamoja na LBL Mtwara Media Company Limited yenye usajili ( na 181289972), LBL Morogoro Media Company Limited yenye usajili ( 179770873) na LBL Geita Advertising Media Limited yenye usajili ( Na 180439242).

Nyingine ni LBL Mbeya Media Limited yenye usajili ( Na 179978326), LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited ( Na 181302259), LBL Mbezi Advertising Media Company Limited ( Na 180582835)
LBL Ubungo Media Limited ( Na 180960333)
na LBL Mabibo Media Company Limited (Na 181117346).

“LBL Mbagala Media Company Limited ( 181248874) LBL Gongo la mboto Media Advertising Company Limited (Na 18151438) na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited Na 18004692,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo msajili alizijulisha Kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya Januari 2-26, 2025, na kwa kuwa kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu cha 400A (2), amezifuta kampuni hizo rasmi kuanzia Februari 27, 2025.

Pia ameutaka umma ufahamu kwamba hakuna sharia wala taasisi yenye mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara ya za upatu hapa nchini na kwamba anaendelea kufuatilia kampuni nyingine zinazofanya shughuli za kibiashara nje ya katiba zao na kinyume cha sharia na taratibu na kusisitiza kwamba ataendelea kuzichukulia hatua stahiki ikiwemo kuzifuta kwenye :Rejista ya Kampuni

Aidha msajili ametoa wito na kuwahimiza wananchi kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka husika juu ya uwepo wa biashara ya upatu, kwani upatu ni kinyume cha sheria za nchi.

Wakazi wa Dar, Pwani na Morogoro kupata Maji ya Uhakika
Prof. Mkenda asisitiza umuhimu wa Elimu ya amali kukuza ujuzi