Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amewataka watumishi wa sekta ya afya kutoa huduma bora zinazoendana na ubora wa miundombinu ambayo serikali imewekeza katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi, ikiwa ni sehemu ya ziara shirikishi ya usimamizi wa upatikanaji wa huduma mbalimbali za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii katika Mkoa wa Dodoma.
“Tuna majengo mazuri na vifaa vyote vya msingi ambavyo vimetolewa na serikali. Hivyo, ubora wa majengo uendane na huduma zinazotolewa kwa kuzingatia miongozo ya afya,” amesema Dkt. Mfaume.
Aidha, amesisitiza kuwa kuna miongozo mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) inayopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Vilevile, amewakumbusha wasimamizi wa miradi ya afya inayoendelea kutekelezwa nchini kuhakikisha kuwa miradi hiyo inazingatia thamani ya fedha ili ikidhi malengo ya serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi.