Watakiwa kuchukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko
6 hours ago
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera, Domina Jeremiah ameitaka Jamii kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na Magonjwa ya mlipuko ikiwemo Marburg.
Domina ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya Afya katika Kanisa la Waadventista Wasabato Ng’ambo, na kudai kuwa miongoni mwa tahadhari muhimu za kuchukua katika kujikinga ni pamoja na kuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.
“Tunasema Kinga ni bora kuliko Tiba hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari, tunawe mikono kwa maji tiririka na sabuni, tusisalimiane kwa kushikana mikono,pia toa taarifa kwa uongozi wa Kijiji, mtaa, Kituo cha Huduma za Afya kilichokaribu nawe au piga 199 bure,” amesema.
Aidha, ametaja baadhi ya dalili za ugonjwa wa Marburg ni kutoka damu mwilini, Homa , kuhara au kuharisha damu na unaweza kuenezwa kwa kugusa majimaji ya mgonjwa ikiwemo jasho, damu, nguo, matandiko ya mtu mwenye maambukizi na kuchangia vitu vyenye ncha kali,maambukizi kutoka kwa wanyamapori ikiwemo sokwe, tumbili.
Mchungaji Samwel Mbilanga ni Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Ng’ambo Wilayani Biharamulo ameishukuru Serikali kwa kuweka jitihada kubwa za Utoaji wa Elimu ya Afya huku akisema Kanisa hilo limejizatiti katika masuala ya Afya.
“Tunashukuru Serikali kwa kuweka Kipaumbele cha elimu ya Afya ambapo na sisi kama Kanisa moja ya jambo kubwa tunalozingatia ni masomo ya Afya kanisani na tumehakikisha kuwa na ndoo za maji tiririka kila lango la Kanisa na chooni, na suala la ulaji huwa tunazingatia sana Afya”amesisitiza.
Aidha, Mchungaji Mbilanga amesema katika kipindi suala la maombi kwa kushikana wamesitisha ili kuzua maambukizi ya magonjwa ya mlipuko, huku baadhi ya Waumini wa Kanisa hilo, akiwemo Marther Nyanjara pamoja Zabron Mfungo wamesema kupitia elimu hiyo watakuwa mabalozi wa kueneza ujumbe kwa waumini wengine hasa kwa kusambaza namba 199 na kuepuka kugusana .
Katika utoaji wa elimu ya Afya kanisani hapo,baadhi ya wadau walioshiriki ni pamoja na Uwakili kutoka UNICEF, Africa CDC na TADIO.