Watu watatu wakiwemo watoto wawili wamenusurika kifo baada ya bati la kanisa la CAG lililopo mtaa wa Gatoya wilayani Bariadi mkoani Simiyu kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa.
Watu hao waliofahamika kwa majina ya Denis Anania(9), Yasin Ismail(8) na Ibrahim Yohana (26) wote wakiwa wakazi wa mtaa huo walifika kanisani hapo ili kujikinga na mvua kabla ya ukuta na paa kuporomoka
Manusura wa ajali hiyo Ibrahim Msangi anasema kuwa kabla ya mvua kuanza walikuwa nje na muda mfupi baada ya mvua kuzidi waliingia ndani ya kanisa hilo ambalo lilizidiwa na kuanguka.

” tulikuwa wengi lakini watoto wengine wakaijiwa na wazazi wao baadae nikaona ukuta umendodoka na kuwaangukia wale watoto waliokuwa wamebaki na mimi ikabidi nianze kuwaokoa kisha nijiokoe na mimi baadae tukaenda hospitali kwa msaada wa majirani “anasema Ibrahim
Askofu wa Kanisa hilo, Yohana Msengi amesema kwasasa hakuna sehemu nyingine ya kuabudia hivyo anawaomba watanzania wasaidie ili wapate sehemu ya kufanya ibada.

“Ibada tulikuwa tunafanya hapa na mimi naamini watanzania wanaupendo sana naomba mtusaidie tupate sehemu ya kuabudia maana hatuna sehemu nyingine,” amesema, Askofu Msengi.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Victoria Vazana amewataka wananchi wa maeneo hayo ambao nyumba zao zinahitaji ukarabati wafanye ukarabati kabla maafa zaidi hayajajitokeza.

“Kila Mwananchi aangalie nyumba yake kama inahitaji ukarabati basi nashauri mfanye hivyo mapema kwa sababu mvua ni baraka na tuliiomba sana lakini tunatakiwa kujiandaa na ili maafa kama haya yasijitokeze,” amesema Victoria.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Muhammed Nkesa ambaye alimuwakilisha Kaimu Kamanda wa Zimamoto Mkoani humo, amesema kuwa hadi sasa hawajapata takwemu halisi za nyumba zilizoezuliwa.

“Tunathibisha kupokea majeruhi hao na kuwapeleka katika Hospitali ya Somanda ambapo wengine waliruhusiwa na wengine bado wanaendelea kupatiwa matibabu lakini hadi kufikia sasa bado hatujapata idadi ya nyumba zilizobomolewa kwa sababu zipo zingine ambazo hazijaanguka ila zimeezuliwa tu mapaa yake,” Kamanda Muhammed.