Mwanaume mmoja, Collins Leitich almaarufu Chepkulei anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano Nchini Kenya, baada ya kufungua kituo haramu cha Polisi katika kijiji cha Cherus, kilichopo Kesses Kaunti ya Uasin Gishu.
Kulingana na taarifa ya Polisi wa eneo hilo, imeeleza kuwa mshukiwa huyo anayejulikana pia kama Chepkulei alifungua kituo cha polisi bila kuwa na ujuzi wala idhini ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Collins Leitich, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Asis katika eneo la Ndugulu, alikuwa ameanzisha kituo hicho bandia na kukipaka rangi rasmi za Polisi, ili kionekane kama halali na mamlaka za Upelelezi zikiendelea kumuhoji nia yake halisi.
Kituo hicho cha doria bandia kiligunduliwa na Polisi wa eneo hilo, ambao walianza uchunguzi mara moja, ambapo Maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Kamuyu, chini ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Kondoo, walifahamishwa na kurekodi tukio hilo chini ya makosa ya jinai namba OB04/08/03/2025.