Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekuwa na ongezeko la kuhifadhi maji kutoka lita 153,649,000 hadi lita 198,965,000 sawa na ongezeko la lita 45,316,000.

Akizungumza na Waandishi wa habari Leo Machi 11,2025 Jijini Dodoma, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire, amesema ongezeko hilo limesaidia Wananchi wa Mkoa huo kuendelea kupata maji kwa wakati bila changamoto.

“DAWASA imeendelea kupata mafanikio mbalimbali moja wapo likiwa hilo la ongezeko la kuhifadhi maji kuongezeka, lakini pia Mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji umeongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kilomita 7,206 sawa na ongezeko la kilomita 2,513.4”, amesema.

“Kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka wastani wa asilimia 89 hadi asilimia 93 na huduma ya usafi wa mazingira kutoka asilimia 25 hadi asilimia 45, Uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita 520,000,000/siku mpaka lita 534,600,000/siku sawa na ongezeko la lita 14,600,000/siku,” amesema.

Hata hivyo amesema DAWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi zaidi ya ishirini na tano (25) yenye thamani ya fedha za Kitanzania Shilingi billioni 987.6.

“Miradi yenye thamani ya Tsh Bilioni 232.9 imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi, Miradi yenye thamani ya Tsh Bilioni 754.7 bado ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, Aidha miradi iliyopo katika mipango ya muda mfupi na mrefu yenye thamani ya Tsh Trilioni 3.1
imebuniwa na iko katika hatua mbalimbali za maandalizi,” amesema.

“Fedha hizo zinajumuisha gharama za usanifu, ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa majisafi, pamoja na ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya ukusanyaji, usafirishaji, upokeaji na uchakataji wa majitaka, Miradi hiyo inatekelezwa kwa kutumia fedha za makusanyo ya DAWASA.

Serikali kuu na mikopo ya masharti nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, wakiwemo Benki ya Dunia, Serikali ya Korea Kusini (kupitia Benki ya Exim ya Korea) na Serikali ya India (kupitia Benki ya Exim ya India),” amesema.

UVCCM Kagera waanzisha Samia New Voters Campaign
Rais Samia ashiriki Mkutano Mkuu wa 39 wa ALAT