Wakuu wa Usalama Barabarani watakiwa kusimamia Sheria
11 hours ago
Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya wametakiwa kuongeza kasi katika usimamizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabani ili kuwadhibiti madereva wanaokiuka sheria hizo na kusababisha ajali za barabarani.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadh
Juma Haji wakati akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Usalama Barabarani
wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania bara na Zanzibar jijini Dodoma.
Alisema kukiwa na usimamizi mdogo wa Sheria za Usalama Barabarani kutasababisha uwepo wa madereva wazembe ambao watakuwa wanaendesha bila kuzingatia sheria wala kufuata taratibu na kanuni za Usalama Barabarani hivyo kusababisha ajali na matokeo yake ni ongezeko la majeruhi na vifo kwa watumiaji wengine wa barabara.
Pia, aliwasisitiza wakuu hao wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya kuwasimamia vema askari walio chini yao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua stahiki wale wanaokiuka maadili ya Jeshi la Polisi kwa kuendekeza rushwa na mengineyo yasiyo na maadili.