Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeiomba serikali kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi na kuwalipa stahiki zao, hususan kwa watumishi wapya, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Lazaro Nyamoga ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua mradi wa Hospitali Mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza ambayo ni miongoni mwa hospitali mpya 129 zilizojengwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

“Suala la watumishi katika baadhi ya mikoa, ikiwemo Kigoma, ni changamoto. Kamati inasisitiza mambo mawili: kuongeza watumishi hasa pale fursa zinapojitokeza, na kuhakikisha malipo stahiki yanatolewa kwa watumishi wapya na wanaohama ili kuwapa moyo wa kufanya kazi kwa bidii,” amesema Nyamoga.

Aidha,Kamati hiyo imetoa maelekezo kwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhakikisha jenereta kubwa linapelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Uvinza, kwani lililopo sasa halina uwezo wa kusambaza umeme kwa hospitali nzima.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Zainab Katimba, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya kamati huku akiwataka watumishi wa umma kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Maisha: Mzungu wa Facebook alivyonitapeli Dola 350
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 13, 2025