Viongozi mbalimbali wanaoshiriki mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi ya nishati endelevu kwa watu wote unaofanyika nchini Barbados wameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa nishati endelevu kwa gharama nafuu.

Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika jijini Bridgetown, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania kwa upande wake chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepanga kuwawezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema, kupitia mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115 utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu kwa maendeleo na ustawi wa wananchi katika ngazi mbalimbali.

Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, utekelezaji wa lengo namba 7 katika mpango wa maendeleo ya milenia unahitaji ushirikiano miongoni mwa Serikali na sekta binafsi katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi ikiwa ni moja ya utatuzi wa changamoto zilizopo.

Amesema ni muhimu kwa mataifa kuwekeza katika miundombinu kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi sambamba na kuweka mifumo ya ubunifu na utashi katika kuwezesha upatikanaji wa nishati kwa usawa bila kuacha makundi mengine.

Naye, Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley amesema ni wakati sasa wa kuweka mkakati wa kimataifa na kukubaliana kushirikiana kumaliza changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa wote.

Akizungumzia mkutano wa misheni 300 (M300) uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mia amesema inatia simanzi kuwa na watu zaidi ya milioni 600 barani Afrika wanaishi bila huduma ya umeme suala ambalo limesababisha changamoto katika nchi nyingi duniani.

“Tunahitaji kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo, uwe ufumbuzi wa ndani au kutoka katika nchi yoyote duniani,” amesema Mottley.

Kwa upande wake, Rais wa Sierra Leone, Mhe. Julius Maada Bio amesema katika kipindi hiki ambapo nishati ni nyenzo muhimu katika upatikanaji wa maendeleo, ni muhimu kuwezesha watu na makundi yote kupata nishati hususani katika maeneo ya vijijini yanayokabiliwa na umasikini uliokithiri.

“Wanawake na watoto ambao wanatumia muda mwingi kutafuta nishati ambayo sio safi kwa ajili ya kupikia, wanatakiwa kuwezeshwa kupata nishati safi na hivyo kutumia muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo,” ameongeza.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mtendaji Mkuu SEforALL, Damilola Ogumbiyi, amesema zinahitajika ajenda madhubuti za kuwezesha kukabiliana na vitendo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo safi.

“ Tumeshuhudia matokeo yanayosababishwa na ukosefu wa nishati safi kama vile uharibifu wa mazingira unaosababisha ukame na mafuriko ambayo kwa kupata nishati safi tunaweza kuondokana nayo,” amesema.

Mkutano huo wa kimataifa ni mwendelezo wa mikutano ya kikanda na kimataifa inayokusudia kupata suluhisho la changamoto zinazotokana na matumizi ya nishati chafu.

Mwezi Januari, 2025, viongozi na wakuu wa nchi mbalimbali barani Afrika na taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika walikutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta uwezekano wa kuwawezesha watu takribani milioni 300 barani Afrika kupata huduma ya nishati ya umeme.

PIC yakagua ujenzi makazi ya Watumishi wa Umma
Kusaga ampa mwaliko maalum Rais Samia kwenye Tuzo za Malkia wa nguvu