Diaspora waahidiwa ushirikiano uchangamkiaji fusra za kiuchumi Nchini
7 hours ago
Watanzania Waishio Ughaibuni wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizoko katika maeneo yao na Serikali itawaunga mkono pale inapohitajika.
Hayo yamesemwa kwa njia ya Mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipofungua Mafunzo ya Ujasiriamali na Uendeshaji wa Biashara ya Kimataifa kwa Watanzania waishio nchini Comoro yaliyoanza leo nchini humo.
Aliwaeleza Watanzania hao kuwa Serikali iko karibu zaidi na Diaspora kuliko Awamu yeyote iliyopita ambapo Sera ya Mambo ya Nje inawatambua rasmi na hivi karibuni utaratibu wa Hadhi Maalum utafikua tamati kwa faida yao.
Awali Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu alimueleza Waziri Balozi Kombo kuwa biashara ya Comoro na Tanzania hivi sasa iko takriban shilingi bilioni 148 kwa mwaka ambayo ni takriban shilingi milioni 405 kwa siku na imekuwa ikiongezeka. Hata hivyo mchango halisi wa ushirikiano wa Tanzania na Comoro ni takriban shilingi bilioni 500 kwa mwaka ukichanganya sekta zote ikiwemo Huduma.
Mafunzo hayo, yanaendeshwa na Chuo cha Uhasibu Arusha ambapo wakufunzi watatu wapo nchini Comoro ambapo Mkuu wa Chuo hicho Prof. Eliamani Sedoyeka alieleza kuwa wakufunzi hao watafundisha Utengenezaji wa Mpango wa Biashara, Uendeshaji wa Biashara ya Kimataifa, Namna ya kukabiliana na Vihatarishi katika Biashara na Utunzaji wa Mahesabu.
Hafla hiyo ya Ufunguzi ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Kitengo cha Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje, Salvatory Mbilinyi na mafunzo hayo yatafanyika kwa siku tatu.