Serikali Nchini, imesema inatekeleza ahadi yake ya ujenzi bora wa nyumba na miundombinu mingine, kwa kuwezesha utengenezwaji wa kanuni ya majengo itakayotumika kwenye ujenzi wa majengo mbalimbali nchini. Akizungumza katika kikao kazi cha kuandaa rasimu ya kanuni hiyo mjini Morogoro, Mbunifu Majengo kutoka katika Chama Cha Wabunifu Majengo nchini (AAT), T’chawi Mike amesema kukamilika kwa uandaaji wa kanuni hiyo kutapunguza kero na athari mbalimbali zinazosababishwa na ujenzi usiozingatia kanuni. Amezitaja baadhi ya athari hizo kuwa ni pamoja na uwepo wa majengo yanayo karibisha majanga, ikiwemo kubomoka au kuanguka, majengo kutokidhi viwango vya ujenzi vinavyoruhusu uokoaji pindi hatari zinapotokea na athari mbaya nyinginezo.
”Uandaaji wa rasimu ya kanuni hizi za ujenzi wa majengo umezingatia viwango vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa, hivyo kutegemewa kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ndogo ya ujenzi wa majengo nchini,” amesema Mhandishi Innocent Johnbosco toka Shirika la Viwango Nchini (TBS). Aidha, Johnbosco alishauri elimu itolewe kwa watumiaji wa kanuni hiyo kabla ya kuanza kuitumia, ili kuepuka matumizi yasiyofaa yanayoweza kusababisha kuendelea kuwepo kwa changamoto za ujenzi wa majengo usio faa na kero nyingine zinazoepukika.
Naye Mbunifu Majengo kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (FRF), Joseph Ngido amesema wako tayari kushiriki kuhakikisha matumizi sahihi ya kanuni hiyo, huku Mhandisi kutoka NCC, Magdalena Hyera akisema uratibu huu unaofanywa na Baraza la Taifa la Ujenzi ni utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria. Utekelezaji huo unafanywa na Wizara ya Ujenzi kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), lenye jukumu la kuratibu na kuandaa miongozo mbalimbali inayotumika katika sekta ya ujenzi, ikiwemo ya Ujenzi wa Majengo kwa kushirikisha wadau wa ujenzi na wataalamu kutoka taasisi za umma na binafsi.

ACT Wazalendo wataka majibu ya Serikali kuzuiliwa kwa Viongozi Angola
Ujenzi wa miundombinu SGR waipaisha TRC