Watendaji Kata wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, wametakiwa kuwahamasisha Wazazi na Walezi kuchangia chakula cha Wanafunzi shuleni, ili kuboresha lishe na utendaji wa watoto darasani.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya lishe hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Masala amesema kuchangia chakula shuleni ni hatua muhimu ya kuwawezeshaWanafunzi kuwa na uwezo mzuri wa kujifunza na kufikiria.
Amesema, “tunapotoa chakula kwa watoto wetu, tunawajengea mazingira bora ya kujikita katika masomo yao, na ubongo wao unapata nguvu ili kuzingatia masomo.”
Masala ameongeza kuwa changamoto ya lishe duni inachangia moja kwa moja kushuka kwa ufaulu wa Wanafunzi na kuathiri maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Aidha, amewahimiza Watendaji Kata hao kuhakikisha kuwa Wazazi na Walezi wanajua umuhimu wa kuchangia chakula kwa watoto wao, ili kupunguza adha za Watoto kutokamilisha masomo kutokana na njaa au udhaifu wa mwili.