Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imewahimiza wasimamizi wa miradi ya kuhifadhi mazingira ngazi ya Halmashauri za Wilaya kuisimamia miradi hiyo kwa ukaribu ili ilete tija kwa wananchi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kutekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi tarehe 17 Machi, 2025.
Mhe. Kiswaga ameongoza kamati hiyo kukagua miradi inayotekelezwa kupitia mradi wa SLR ambayo ni josho, banio, birika itakayosaidia kuogesha, kunyweshea na kutibu mifugo, pia mradi wa ng’ombe wa maziwa waliotolewa kwa kikundi ili kusaidia wananchi kuachana na shughuli za uharibifu wa mazingira na mradi wa shamba darasa la malisho lenye ukubwa wa ekari 2.5, miradi iliyopo katika Kijiji cha Kapanga yote ikiwa na thamani ya shilingi milioni 81.
Amesema Serikali Kuu inapeleka fedha katika halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi hivyo wasimamizi wa miradi ngazi ya chini wanapaswa kuisimamia ili ikamilike kwa wakati uliopangwa na kunufaisha wananchi sanjari na kulinda mazingira.
“Ndugu zangu miradi hii ni ya kwenu wananchi Ofisi ya Makamu wa Rais inahakikisha fedha za utekelezaji zinawafikia na hivyo ninyi watu wa Halmashauri hadi ngazi ya vijiji mnalo jukumu la kufuatilia utekelezaji wake kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha zilizotengwa,“ amesisitiza Kiswaga.
Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibiwa miradi ambayo inasaidia katika kuhifadhi mazingira na kusema ni muhimu elimu iendelee kutolewa kwa wananchi sanjari na uwepo wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amewahimiza wasimamizi wa miradi ngazi za wilaya kukamilisha miradi kwa wakati uliopangwa ili wananchi waweze kunufaika.
Amesema malengo ya miradi hii ni kuwabadilisha wananchi kutoka kwenye shughuli za uharibifu wa mazingira hivyo wanapopelekewa miradi na kukamilishiwa kwa wakati wataachana na shughuli za uharibifu wa mazingira.
Aidha, Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri wa kusimamia fedha kwa ukamilifu walizopokea kutoka Serikali Kuu katika kutekeleza miradi iliyokusudiwa ili matokeo yaonekane na kuomba zingine kama kuna uhitaji.
Awali akiwasilisha taarifa za miradi iliyotembelewa na kamati, Mratibu wa Mradi wa LSR Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Ephraim Luhwago ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha halmashauri kupata mradi huo ambao una manufaa makubwa kwa wananchi.
Amesema kjuwa lengo kuu la mradi ni kuimarisha usimamizi wa pamoja wa ardhi iliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo ikolojia na jamii kwa ujumla.
Viongozi walioambatana na kamati katika ziara hiyo ni hiyo ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme na Watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mradi wa SLR wenye thamani ya sh. bilioni 25.8 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais unatekelezwa Halmashauri za wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi), Iringa (Iringa), Mbeya, Mbarali (Mbeya) na Sumbawanga (Rukwa).