Kiasi cha TZS bilioni 2.7 kwa ajili ya kuimarisha ofisi saba za kanda za Shirika la Viwango Nchini – TBS katika Mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Mbeya.
Akizungumza hii leo Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Nchini, Dkt. Ashura Katunzi amesema shirika limejipanga kuwa na ofisi za mipakani ikiwemo Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili na Tarakea.
Nyingine ni Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Bandari ya Bagamoyo, bandari ya Mbweni, bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere – Dar es Salaam na Bandariya Tanga.

Amesema, TBS imeweza kutoa mafunzo kwa jumla ya wadau 5,052 wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani nawasindikaji.
“Mafunzo hayo yalihusu dhana nzima ya viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na yamewawezesha kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti ubora, hivyo kuwaandaa kuhimili ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa”, amesema
“Pia kupitia Mradi wa Qualitan TBS na SIDO mwaka 2024waliwezeshwa kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula 1000 katika mikoa 10 (Dar es Salaam, Singida, Mwanza, Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Tanga, Ruvuma na Kilimanjaro”. Amesema Dkt. Katunzi.
Vilevile amesema TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora.

“Njia hizo ni pamoja na kushiriki katika makongamano, maonesho, warsha na semina, kuandaa mikutano na wadau wa masuala ya viwango, kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama na kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya.”
“Aidha, elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari zikiwemo redio jamii, redio za kitaifa, runinga, magazeti, mitandao ya kijamii, matangazo, majarida na vipeperushi”. Amesema Dkt. Katunzi