Wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao bado hawajafikiwa na huduma ya umeme wameiomba Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi ya kuwaunganishia umeme katika kaya zao ili waweze kuutumia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Hayo yameelezwa kupitia Viongozi wa Vijiji vya Melela, Mtwango, Lwangu, Lupende na Melela wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyolenga kukagua maendeleo ya mradi wa usambazaji umeme vijijini katika vijiji vya Mkoa wa Njombe tarehe 18 Machi 2025.

Viongozi hao wamesema wananchi wameingia hamasa zaidi ya kuunganishiwa umeme baada ya kuona maendeleo yanazidi kuimarika katika baadhi ya Kaya ambazo tayari zimeunganishiwa umeme.

Aidha, wameishukuru Serikali ambayo imetoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ukiwemo umeme katika maeneo yao ambapo kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakiona kasi kubwa ya maendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewatoa hofu wananchi hao kwa kuwaeleza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha inafikisha umeme kwa wananchi wote ifikapo 2030.

Ameeleza kuwa maendeleo katika maeneo yote hupelekwa kwa hatua kama ilivyo kwa miradi ya umeme lakini lengo la Serikali ni wananchi wote wafikiwe na huduma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David amewasisitiza wananchi kuendelea kutandaza nyaya katika nyumba zao ili miradi ya umeme uiakapowafikia waunganishwe kwa haraka.

Ameeleza kuwa, wananchi ambao hawahitaji kusuka nyaya wafike katika ofisi za TANESCO Ili wapatiwe kifaa cha umeme tayari( UMETA) kwa gharama ya Shilingi elfu 27,000 tu.

Maeneo ya kijamii yamepewa kipaumbele kufikiwa na Umeme - Kapinga