Upatikanaji wa mbolea Nchini, umeongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024 huku Wafanyabiashara wa Mbolea waliopewa leseni nao wakiongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 kufikia 7,302 Februari, 2025.
Hayo yamebainishwa mbele ya Waandishi wa Habari hii leo Machi 17, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent ambaye amedai pia Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Mbolea na Afya ya Udongo (2024 – 2030) ambao tayari umeanza kutumika.
Amesema, “biashara ya mbolea nchini imekua kwa kiasi kikubwa ambapo upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024” amesema.
Laurent amesema, matumizi ya mfumo wa kidijitali katika kusambaza mbolea ya ruzuku umeinufaisha Serikali hususani katika kuwezesha kuanzisha kanzidata ya kuaminika ya wakulima, Mawakala wa mbolea, Waingizaji na Wazalishaji wa mbolea Nchini.
“Mfumo huu wa kidijitali umekuwa nyenzo muhimu ya ufuatiliaji na uendeshaji wa biashara ya mbolea nchini kuanzia mbolea inavyoingizwa au kuzalishwa kwenye viwanda vya ndani hadi inapouzwa kwa mkulima katika maeneo mbalimbali nchini,” aliongeza Laurent.
Aidha, amesema mfumo huo umerahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za matumizi ya mbolea nchini pamoja na kudhibiti udanganyifu katika mpango wa ruzuku ya mbolea na kwamba wameweka malengo na mbinu za kuhakikisha upatikanaji, ufikiaji na matumizi ya mbolea kwa wakulima unakuwa ya uhakika.
Mamlaka hiyo pia imeanzisha Maabara ya kisasa ya mbolea, Tanzania inakuwa Nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Maabara mahususi ya mbolea yenye uwezo wa kupima sampuli za mbolea, udongo na tishu za mimea.
“Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha udhibiti wa ubora wa mbolea nchini,
Aidha, maabara hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania, kama vile Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, na Rwanda,” amesema Laurent.