Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameelekeza juhudi iongezwe katika kudhibiti upotevu wa maji.
Amesema hayo akizindua Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Maji kwa Mwaka 2023/24 jijini Dar es salaam.
Dkt. Biteko amesema hatua hiyo ni muhimu kwasababu mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji.

Ameainisha kuwa suala la upotevu wa maji katika mamlaka za maji lina sura tofauti na sio miundombinu pekee bali kuna hujuma za wizi hivyo ifanyiwe kazi mapema na kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi.
Amesema hatua kubwa imefanyika katika Sekta ya Maji, na hakuna anayebisha ila nguvu zaidi inahitajika.
Dkt. Biteko ametaja mamlaka ambazo zimepiga hatua katika kudhibiti upotevu wa maji ni pamoja na Nzega, KASHWASA, Maganzo na Biharamulo.

Ameongeza kuwa kudhibiti upotevu wa maji kutaleta faraja kwa wananchi kwasababu lengo ni kila Mtanzania kupata huduma ya maji.
Ameongeza kuwa suala la usafi wa mazingira kwa afya ya wananchi lipewe kipaumbele katika kutoa huduma.
Amesema maji ni kiungo muhimu katika maisha ya kila siku na juhudi iongezwe katika uzalishaji.

Mamlaka zilizofanya vizuri zenye wateja zaidi ya elfu ishirini ni pamoja na Moshi, Iringa na Songea.
Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Maji kwa mwaka 2023/24 ni muendelezo wa kuangalia utendaji ikiwa ni ya 16.