Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu watatu waliokamatwa wakiwa na gramu 3,263.72 za Dhahabu yenye thamani ya Sh749,509,531.94 wakisafirisha kwa njia za magendo kwa kutumia gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajiri T. 739 EEH mali ya Emmanuel Kidenya wa Kahama.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amesema waliokamatwa ni Yohana Idama (34), Mkazi ya Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela Mwanza, Moshi Manzili (26), Mkazi wa Bariadi Simiyu na Hamidu Salumu (25), Mkazi wa Nyasubi Wilaya ya Kahama Shinyanga.

Ameongeza kuwa Watuhumiwa hao wamekamatwa Machi 24, 2025 majira ya saa 5 usiku katika Mtaa wa Kapera uliopo Wilayani Bukombe, baada ya Jeshi la Polisi kupata Taarifa za Siri na kuweka mtego uliofanikisha na baada ya upekuzi walikutwa wakiwa na kiasi hicho cha Dhahabu.
Uchunguzi wa Tukio hili kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine unaendelea kufanyika sambamba na kubaini na kuwakamata watakao bainika kujihusisha watafikishwa Mahakamani.