Kiungo wa klabu ya Southampton ya nchini England Sofiane Boufal, ameongeza pigo katika kikosi cha timu ya taifa ya Morocco ambacho kinajiandaa na fainali za Afrika kwa mwaka 2017.
Sofiane ambaye alikua sehemu ya kambi ya timu ya taifa ya Morocco iliopo huko falme za kiarabu, amelazimika kuondolewa kwenye mipango ya kocha Hervé Renard, kufuatia kukabiliwa na majeraha.
Tayari amesharuhusiwa kurejea nyumbani Morocco kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
“Sofiane Boufal ameondoka kambini baada ya kufanyiwa vipimo na kubainika hayupo fit kwa ajili ya fainali za Afrika zitakazoanza mwishoni mwa juma hili nchini Gabon,” imeeleza taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka soka nchini Morocco FRMF.
Sofiane anakua mchezo wanne kupata majeraha akiwa katika kambi ya maandalizi, akitanguliwa na Younes Belhanda aliyevunjika kidole, Oussame Tannane anaesumbuliwa na majeraha ya paja pamoja na Nouredine Amranat anaekabiliwa na maumivu ya kifunzo cha mguu.
Kikosi cha Morocco kinatarajia kucheza mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Finland hapo kesho, na kitatupa karata yake ya kwanza katika fainali za Afrika kwa kupambana na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mjini Oyem Januari 16.