Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amewashuri wataalamu wa kilimo nchini kuwapa maelekezo mazuri wakulima ili wapate maelekezo ya kutosha badala ya kuwashawishi watumie mbegu za kisasa.
Mghwira amesema kuwa mbegu nyingi za kisasa zinazo tengenezwa viwandani hazina ubora hata wa kuishi misimu miwili ya kilimo, hivyo kufanya wakulima kulazimika kununua mbegu kila msimu wa kilimo unapofika.
“Tatizo nchini kwa sasa ni wataalamu kulazimisha wakulima watumie mbegu za kisasa za viwandani ambazo hazina ubora unatakiwa hivyo ni vyema tukatumia mbegu za asili,”amesema Mghwira.
Aidha, kwa mujibu wa mgombea huyo wa urais huyo wa mwaka juzi , amesema kuwa alifanya utafiti kuhusu usalama wa chakula na kubaini kwamba wataalamu wanatakiwa kufanya utafiti wa kutosha na kuwapa ufumbuzi wakulima kuhusu namna ya kulima na na kupanda mbegu za asili bila matatizo.
Hata hivyo Mghwira amewanyooshea kidole wananchi kuhusu hali ya mabadiliko ya tabia nchi, akisema wanahusika pakubwa katika uharibifu huo wa kukata miti hovyo.