Timu ya Simba usiku wa kuamkia hii leo ilifanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ya michuano ya kombe la Mapunduzi kisiwani Unguja kwa kuifunga Young Africana katika mchezo wa hatua ya nusu fainali.
Simba walitimiza mpango wa kuingia fainali, kwa changamoto ya mikwaju ya penati nne kwa mbili, baada ya dakika 90 kumalizika na magwiji hao wa soka la bongo walishindwa kufungana.
Kutokana na ushindi huo, afisa habari wa klabu ya Ruvu Shooting ambayo ilipoteza mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Simba siku chache kabla ya kuanza michuano ya kombe la Mapinduzi, Masau Bwire ametuma salamu za pongezi kwa Wanamsimbazi.
Masau ametuma ujumbe huu kwa Wanamsimbazi kupitia mitandao ya kijamii:
Niungane na Watanzania wengine, Wadau, Wapenzi na Washabiki wa Soka, kuwapongeza Simba ya Dar es Salaam kwa kufanikiwa kuingia hatua ya fainali ya mashindano ya kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Yanga pia ya Dar es Salaam katika hatua ya nusu fainali kwa magoli 4 kwa mawili, yote yakipatikana kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa suluu.
Haikuwa rahisi kwa Simba kupata matokeo hayo kutokana na uimara wa timu ya Yanga, ndiyo maana dakika 90 za mchezo zikayeyuka patupu, hakuna kati ya wawili hao aliyefanikiwa kumtoboa mwenzake japo kitobo cha kizushi mwamuzi akakikataa, nyavu za pande zote, ndani ya dakika 90 zilikuwa salama kama Malikia wa mchwa ndani la bonge la kichuguu!
Lakini kwakuwa wakati fulani binafsi naamini kuwa matokeo ya mpira wa miguu utambaa na bahati, bahati, tena ya mtende jana ikadondoka katika Sharabu za Simba mwenye meno chonge, ikawa kazi nyepesi kwake kutia kinywani na kutafuna kiubwete kabisa tende hizo za Jangwani!
Yanga, msiumie sana, hii ni kawaida! Ni sawa na mwanamume anayeachwa na mchumba, hujipanga na kutafuta mchumba mwingine na kuoa!
Kikombe cha Mapinduzi ni mchumba umenyang’anywa, ukilia sana, ukasononeka na kuugua moyo eti umepokwa mchumba, wanaume wenzako tutakucheka ujinga! Changamka, anza maandalizi ya kuchumbia mwingine mwisho wa siku, kama umekamilika utaoa!
Hongera sana Simba, hatua nzuri mmeifikia na sasa mkisubiri kukutana na jamaa wale wanaotulambisha vitu vitamu ambao mfupa mliourarua kwa shida, taabu na machozi kibao yaliyochafua sharubu zako kwa kiasi fulani, Yeye kwake ilikuwa kama mdondo, hakuhangaika wala kutumia jasho kuuteketeza, aliulamba kirahisi sana, mara Nne kama treni ya Mwakyembe inayofanya safari, kutwa mara Nne Jijini Dar es Salaam!
Katika mchezo wa fainali nimpongeze mshindi atakayeshinda kati yenu mnaoshindana. Hongera sana mshindi na bingwa wa kombe la Mapinduzi mwaka 2017!