Klabu ya Atletico Madrid ipo kwenye wakati mgumu wa kuhakikisha inambakisha mshambuliaji wake wa pembeni kutoka nchini Ubelgiji Yannick Ferreira Carrasco, katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Hofu kwa Atletico Madrid inaendelea kutawala, kufuatia mipango inayoandaliwa na klabu nne za ligi kuu ya soka nchini England, kwa ajili ya uhamisho wa Carrasco ambaye alifunga bao la kusawazisha wakati wa mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita dhidi ya Real Madrid.
Chelsea, Arsenal, Manchester United na Manchester City zinatajwa kuwa katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23.
Klabu nyingine ambao zinatajwa kuwa katika mikakati ya usajili wa Carrasco ni PSG ya Ufaransa na FC Bayern Munich ya Ujerumani.
Hata hivyo Carrasco bado ana mkataba na klabu ya Atletico Madrid hadi mwaka 2022, na kama itatokea anaondoka katika kipindi hiki au mwishoni mwa msimu huu, ada yake ya usajili inakadiriwa kufikia Euro milioni 100.