Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua SACCOS ya Melinne mjini Zanzibar yenye mtaji zaidi ya shilingi bilioni moja.
Majaliwa amefanya uzinduzi huo kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu Zanzibar.
Majaliwa amewataka viongozi wa SACCOS hiyo kuhakikisha wanakuwa wawazi na kutoa taarifa za hesabu za umoja huo kila wakati ili wanachama waweze kuwa na takwimu sahihi.
Amesema viongozi hao wanatakiwa kuwa wawazi kwa wanachama wenzao jambo ambalo litawajengea uaminifu hivyo kuwezesha umoja huo kudumu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa, vyama vingi vya ushirika nchini vimekufa kutokana na viongozi wake kutokuwa waaminifu hivyo Serikali hatokubali kuona suala hilo linatokea katika umoja huo kwani litakwamisha maendeleo.
Pamoja na hayo, Majaliwa amewapongeza wananchi hao kwa kuanzisha SACCOS hiyo kwani wameweza kutimiza ndoto ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ya kuondokana na umasikini, dhuluma na unyonge.
Amesema SACCOS hiyo itawawezesha baadhi ya wanachama kuanzisha miradi ya ujasiriamali na wengine kuongeza mitaji hivyo kukuza biashara zao na kuondokana na umasikini.
Aidha, Majaliwa amewataka wanachama hao kuendeleza mshikamano wao na kuendelea kushirikiana na Serikali ambayo imejipanga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo ya ujasiriamali hasa kwa walio katika vikundi vya uzalishaji.
Pia, amewashauri wanachama wa umoja huo kufikiria uwezekano wa kuanzisha viwanda ili kukuza mitaji yao na kuwezesha umoja wao kuongeza za fursa za ajira nchini.