Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameyaonya baadhi ya magazeti yanayoandika habari za uchochezi na kupotosha wananchi kwa kuwa ni hatari kwa amani ya nchini.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akikagua na kufungua Kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga.
Aidha, Rais Magufuli amesema Serikali haitayavumilia magazeti hayo kama yataendelea kuandika habari za uchochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya nchi kama ilivyotokea katika nchini ya Rwanda na kupelekea mauaji ya kimbari nchini humo.
“Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti ambayo yanafanya mambo ya uchochezi, hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la maneno ya uchochezi chini ya utawala wangu hilo halitakuwepo, kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao ni kuchochea tu ikizungumzwa habari hii wao wanaigeuza, nasema wanisikie siku zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia wasisikie lakini magazeti na vyombo vingine wanafanya uchambuzi vizuri,”amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema uwepo wa amani nchini ndio uliowezesha wawekezaji wa Kiwanda cha Fresho cha kutengenezea mifuko ya kubebea bidhaa za chakula nchini na kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga kujengwa mkoani hapo kwani bila amani visingeweza kujengwa.
Aidha ameitaka Benki ya Uwekezaji Nchini TIB na Taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika viwanda badala ya kuwakopesha wanasiasa ambao hutumia fedha wanazokopa kwa matumizi yasiyowanufaisha watanzania waliowengi
Rais Magufuli ameupongeza uongozi wa mkoa wa Shinyanga kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kutaka Tanzania ya viwanda kwa kujenga viwanda vingi mkoani humo ikiwa ni pamoja na viwanda hivyo viwili alivyovizindua katika siku yake ya mwisho ya ziara mkoani Shinyanga.