Muigizaji na muongozaji wa kipindi cha Vioja Mahakamani kinachorushwa na kituo cha runinga cha KBC cha Kenya, Alliwah amefunguka kuhusu sanaa ya maigizo nchini humo akilinganisha na hali ilivyo nchini Tanzania.
Alliwah alieleza kuwa Steven Kanumba (Marehemu) ni jina lisilofutika katika anga ya maigizo ya filamu nchini Kenya kama mfano mkubwa wa kuigwa kuwahi kutokea kwa vijana wa ukanda Afrika Mashariki, miaka ya hivi karibuni.
“Kanumba ni mfano wa mtu ambaye alikuwa ameamini kwamba sanaa haiwezi kuuawa. Uwe unasapotiwa au uwe hausapotiwi, sanaa ni kitu ambacho hakuna mtu atakayewahi kukisimamisha [kisiendelee],” aliiambia Dar24.
“Kenya huwa tunasema kama Kanumba angekuwa hai leo, kama aliweza kuvuta wasanii kutoka Nigeria kuja Tanzania…. huo ndio moyo ambao hata Kenya tunakosa,” Alliwah alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa wapo wasanii wa Tanzania ambao Kenya bado inawaangalia kwa karibu kutokana na uwezo wao mkubwa wa kuigiza pamoja na stori nzuri akiwemo Lulu na msanii Mkongwe, Mzee Majuto.
Kadhalika, katika upande wa mashairi, Mrisho Mpoto aliyemtaja kuwa ni rafiki yake aliyewahi kufanya nae sanaa nchini Kenya anaheshima kubwa nchini humo tutokana na uwezo wake wa kughani na kuandika mashairi yenye ujumbe wa aina yake.
Akizungumzia tofauti kati ya sanaa ya maigizo Kenya na Tanzania katika hali ya haki miliki na kipato, alisema kuwa tofauti ni kuwa wasanii wa Kenya hulipwa mirabaha kwa kila kazi wanayoifanya kwa kurushwa kwenye kituo chochote cha runinga.
Alisema kuwa kuna chombo maalum cha Serikali kinachofuatilia kazi za wasanii zinavyochezwa kwenye vyombo vya habari kisha kukusanya mirabaha yote kisha kumlipa kila msanii. Kwa hali hiyo, sanaa ya maigizo Kenya imekuwa kazi rasmi ya wasanii.