Bao lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Montenegro Stevan Jovetić katika mchezo wa ligi ya nchini Hispania usiku wa kuamkia hii leo, lilisitisha rekodi ya mabingwa wa soka duniani klabu ya Real Madrid ambao walikuwa wamecheza michezo 40 bila kufungwa tangu mwanzoni mwa mwaka 2016.
Jovetić ambaye amesajiliwa kwa mkopo na klabu ya Sevilla akitokea Inter Milan ya nchini Italia, alifunga bao hilo la ushindi katika dakika ya 90 baada ya nahodha na beki wa Real Madrid Sergio Ramos kutangulia kujifunga katika dakika ya 85.
Mchezo huo uliounguruma kwenye uwanja wa Ramon Sanchez Pijuan, ulishuhudia Real Madrid wakitangulia kupata bao la kuongoza katika dakika ya 67 kupitia kwa mchezaji bora duniani Cristiano Ronaldo.
Real Madrid tangu ilipoanza kunolewa na meneja kutoka nchini Ufaransa Zinedine Zidane, ilikua haijawahi kupoteza mchezo hata mmoja katika michuano yote waliyocheza.
Hata hivyo kupotea kwa mchezo wa usiku wa kuamkia hii leo hakujawaondolea Real Madrid heshima ya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ya nchini Hispania, kwani mpaka sasa wanaongoza kwa kuwa na point 40, huku wakisaliwa na mchezo mmoja mkononi.
Nafasi ya pili inashikwa na Sevilla waliofikisha point 39, wakifuatiwa na FC Barcelona wenye point 38 na nafasi ya nne inakamatwa na Atletico Madrid wenye point 34.
Matokeo ya michezo mingine ya ligi ya nchini Hispania iliyochezwa jana:
Valencia 2 – 1 Espanyol
Celta Vigo 1 – 0 Alaves
Granada 1 – 1 Osasuna
Sporting Gijon 2 – 3 Eibar