Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limetangaza matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne, ambapo wavulana wameendelea kufanya vyema.
Aidha, katika matokeo hayo, mkoa wa Mtwara umeshika nafasi ya mwisho kitaifa baada ya shule tisa kati ya kumi zilizofanya vibaya zaidi katika mtihani wa kidato cha pili kutoka mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde, amesema kuwa matokeo hayo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 93.3 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka jana.
“Idadi inaonyesha kuwa watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu ni 178,115 sawa na asilimia 43.55, wasichana wakiwa 78,466 sawa na asilimia 37,45 na wavulana wakiwa 99,649 sawa na asilimia 49.97,”amesema Dkt. Msonde.
Msonde amezitaja shule zilizoongoza kwenye mtihani wa kidato cha pili kuwa ni St. Francis Girls (Mbeya), Kilimanjaro Islamic (Kilimanjaro), Kaizirege Junior(Kagera), Canossa (Dar es salaam), Twibhoki (Mara), na shule ya wavulana Tengeru (Arusha), Precious Blood (Pwani), Thomas More Mchrinas (Dar es salaam) na Shule ya wavulana Shamsiye (Dar es salaam).
Hata hivyo amezitaja shule kumi zilizofanya vibaya ni Chingunge, Malocho, Michiga, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukokota zote za mkoani Mtwara ikifuatiwa na Nyelo ya mkoani Tanga.