Siku mbili baada ya kusheherekea siku yake ya kuzaliwa, mlinda mlango mkongwe wa timu ya taifa ya Misri Essam El Hadary, leo huenda akaandika rekodi mpya katika fainali za Afrika (AFCON 2017) zinazoendelea nchini Gabon.
El Hadary mwenye umri wa miaka 44, endapo atacheza hii leo atakua mchezaji pekee mwenye umri mkubwa kucheza fainali za Afrika tangu zilipoanzishwa miaka 60 iliyopita.
Kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na gwiji wa soka kutoka nchini Misri Hossam Hassan Hussein ambaye kwa mara ya mwisho alicheza fainali za Afrika mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 40.
Hossam Hassan Hussein
Rekodi nyingine ambayo itaandikwa na El Hadary ni kucheza fainali za Afrika kwa mara ya saba, ambapo awali rekodi hiyo ilikua inashikiliwa na nahodha na beki wa zamani wa Cameroon Rigobert Song.
Rigobert Song
Kikosi cha Misri hii leo kitatupa karata yake ya kwanza katika fainali za AFCON 2017, kwa kucheza dhidi ya Mali katika mchezo wa kundi D.