Waziri wa Viwanda, Biashara na uwekezaji, Charles Mwijage ameiagiza bodi mpya ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kuhakikisha kasi ya uanzishwaji wa viwanda nchini inatekelezeka.
Aidha, ameitaka bodi hiyo kudhibiti kasi ya uuzaji wa malighafi nje ya nchi na kutoa elimu ya uanzishwaji wa viwanda kwa wajasiliamali na wafanyabiashara wadogo ili kufikia lengo la mapinduzi ya viwanda.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizindua bodi hiyo mpya ya Tantrade na kusisitiza azma ya serikali kuanzisha viwanda nchini kwaajili ya kukuza uchumi.
“Muhimu kuhakikisha tunapunguza kasi ya uuzaji wa malighafi nje ya nchi, bidhaa nyingi zitengenezwe hapa nchini hapa nchini na zipelekwe nje, hiyo ndio maana ya Tanzania ya viwanda,uwezo huo tunao na bodi iwajibike ipasavyo,”amesema Mwijage.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo mpya Mhandisi Christopher Chiza, ameahidi bodi itafanya kazi kwa kuzingatia maadili na wajibu wa sheria ya mwaka 2009, ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ili kutimiza malengo yake.