Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini katika kutoa habari kwa ajili ya kuhabarisha umma kuhusiana na mambo mbalimbali yahusuyo Serikali katika kutekeleza majukumu yake.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye alipotembelea na kujionea utendaji kazi wa Kampuni ya IPP Media kwenye vituo vya Televisheni vya ITV, EATV na Capital Tv pamoja na Sahara Media kwa tawi la Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Nape ameahidi kuendeleza ushirikiano baina ya Serikali na vyombo vya habari katika utoaji wa habari ambazo ni muhimu kwa wananchi kujua zikiwemo hatua ambalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kutekeleza majukumu yake katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Niseme kwa kipindi cha nyuma kumekuwa na urasimu wa utoaji wa taarifa muhimu kutoka kwetu kuja kwenu vyombo vya habari lakini niwahakikishe kuwa sasa Serikali imefungua milango kwenu na tuendelee kushirikiana katika kuhabarisha umma wa watanzania,” Amesema Nape.
Kawa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abass amevihakikishia vyombo vya habari nchini ushirikiano mzuri katika kupata habari za Serikali kutoka katika vitengo vyote vya Mawasiliano Serikalini.
Aidha Mkurugenzi wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Vyombo vya Habari vya binafsi nchini katika kutoa taarifa kwa umma ambazo zimesaidia kuelimisha, kuburudisha na kutengeneza mazingira ya watu kuamini yale yanayotolewa na vyombo vyao.
Naye Mkuu wa Sahara Media kwa upande wa Dar es Salaam, Cyprian Musiba ameipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa vyombo vya habari nchini na kuahidi kuongeza ushirikiano baina yao na Serikali katika upashanaji habari.