Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amefanya mazungumzo ya kutafuta suluhu na mshambuliaji Diego Costa, baada ya kutokea malumbano baina yao mwishoni mwa juma lililopita.
Kituo cha televisheni cha Sky Sports kimeripoti kuwa, wawili hao walikutana na kuzungumza faragha katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea ulioopo maeneo ya Cobham jijini London.
Mazungumzo hayo yalifanyika kabla ya mazoezi ya jana, hali ambayo iliibua hisia tofauti kwa maafisa na wachezaji wa klabu hiyo, kutokana na sintofahamu zilizokua zimejitokeza baada ya Conte kubwatukiana na Costa.
Dakika chache baada ya mazungumzo ya meneja huyo kutoka nchini Italia dhidi ya Costa, mshambuliaji huyo aliungana na wachezaji wenzake waliokua wamefika mazoezini na alionekana akiwakumbatia wasaidizi wa benchi la ufundi.
Conte alibwatukiana na Costa kwa kile kinachodaiwa kuwa, ni mkanganyiko wa usajili, ambapo mshambuliaji huyo alikua akilazimisha suala lake la kutaka kuondoka Stamford Bridge na kutimkia nchini China kujiunga na klabu ya Tianjin Quanjian.
Kwa mantiki hiyo sasa Costa anatarajiwa kurejea katika kikosi cha kwanza cha Chelsea mwishoni mwa juma hili katika mchezo wa ligi ya PL dhidi ya Hull City, baada ya kukosa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Leicester City.
Kurejea kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, kutaongeza chachu ya kuwania tuzo ya ufungaji bora kwa msimu huu katika ligi ya nchini England.
Costa anaongoza katika orodha ya wapachika mabao katika ligi hiyo, ambapo mpaka sasa ameshafunga mabao 14, akifuatiwa na Zlatan Ibrahimovic wa Manchester United na Alexis Sanchez wa Arsenal.