Ndege ya jeshi la Nigeria imeshambulia kwa mabomu kimakosa kambi ya wakimbizi katika mpaka wake na Cameroun na kuua watu takribani 52.
Jeshi hilo limekiri kufanya shambulizi hilo kimakosa wakati linalenga kundi la kigaidi la Boko Haram katika vita wanayoiita ‘ya mwisho dhidi ya Boko Haram’. Jeshi hilo limeomba radhi kwa madhara yaliyojitokeza. Shirika la msaada la MSF limesema kuwa takribani watu 200 wamejeruhiwa.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu.
Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi la Nigeria kukiri kufanya shambulizi kimakosa dhidi ya watu wasio na hatia.
Msemaji wa Red Cross, Aleksandra Mtijevic amesema kuwa mbali na wafanyakazi sita wa shirika hilo waliokufa, kundi la watu waliokuwa wakitolewa kusambaza chakula ni miongoni mwa waliojeruhiwa.