Serikali imepanga kutumia bilioni 15 kuwapatia vijana stadi za kazi zitakazo wawezesha kujiajiri na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda.
Hayo yamesemwa mapema hii leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ally Msaki, wakati wa kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar es saalam (DIT) na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Aidha, Ally Msaki amesema kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuiwezesha Taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa vijana hasa ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na ngozi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Vijana 1000 wataanza kupata mafunzo mwezi Februari mwaka huu na yatakayohusu utengenezaji wa bidhaa za ngozi na program hii ipo ndani ya mpango wa miaka mitano.” Amesema Msaki.
Mafunzo hayo ya stadi za kazi kwa vijana yatagharamiwa na Serikali na yatahusisha vijana walio katika mfumo rasmi na wale wasio katika mfumo rasmi wa elimu lengo likiwa ni kuwakwamua vijana ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof. Preksedis Ndomba amebainisha kuwa Taasisi hiyo imejipanga vyema kuwawezesha vijana kwa kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko na kuweka msisitizo katika mafunzo kwa vitendo.