Wababe wa soka kutoka mji wa Madrid nchini Hispania Real Madrid, wameendelea kuwa mdebwedo katika mchezo wa pili mfululizo tangu walipovunjiwa rekodi yao ya kushinda michezo 40.
Mwishoni mwa juma lililopita Real Madrid walipoteza mchezo wa ligi ya nchini Hispania dhidi ya Sevilla kwa kufungwa mabao mawili kwa moja, hali ambayo iliwashangaza wadau wengi wa soka duniani ambao waliamini huenda rekodi ya ushindi mfululizo ingeendelezwa kwa magwiji hao.
Usiku wa kuamkia hii leo, Magwiji hao wa mji wa Madrid walikubali kisago cha pili kutoka kwa Celta de Vigo katika mchezo wa kombe la Mfalme (Copa del Rey), kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.
Celta de Vigo walitanguliwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa Lago Aspas katika dakika ya 64, lakini Real Madrid walisawazisha baada ya beki wao wa pembeni kutoka nchini Brazil Marcelo kumsalimu mlinda mlango Sergio Álvarez dakika ya 69.
Bao hilo la kusawazisha halikudumu, kwani dakika ya 70 Celta de Vigo walipata bao la pili na la ushindi lililofungwa Johny Castro.
Hata hivyo Real Madrid bado wana nafasi ya kulipiza kisasi katika mchezo wa mkondo wa pili wa kombe la Mfalme ambapo watakutana tena na Celta de Vigo Januari 25.
Mchezo mwingine wa kombe la Mfalme uliochezwa usiku wa kuamkia leo, ulishuhudia Alcorcon wakishindwa kufurukuta nyumbani kwa kukubalia kufungwa na Alaves mabao mawili kwa sifuri.
Leo michuano hiyo inaendelea tena:
Atletico Madrid Vs Eibar
Real Sociedad Vs FC Barcelona