Wakati nchi za Afrika Magharibi zikijiandaa kumng’oa kijeshi Rais wa Gambia, Yahya Jammeh anayeng’ang’ania madaraka licha ya kushindwa katika uchaguzi, Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo, Ousman Badjie ametoa msimamo wa kutojihusisha na vita hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, Mkuu huyo wa Majeshi amesema kuwa kinachoendelea nchini humo ni mgogoro wa kisiasa hivyo hataweza kuiingilia kijeshi kwakuwa anawapenda wanajeshi wake.
“Hatutajihusisha kijeshi na kitakachofanyika, huu ni mgogoro wa kisiasa,” alisema. “Sitaweza kuwaingiza wanajeshi wangu kwenye vita ya kipuuzi. Nawapenda watu wangu,” AFP inamkariri.
Kikosi cha jeshi la Senegal kiko katika mpaka wa Gambia kikisubiri kupewa amri kuingia nchini humo kumng’oa Jammeh.
Nigeria na nchi nyingine za Afrika Magharibi zinaunga mkono hatua za kijeshi za kumuondoa kwa nguvu Jammeh.
Jammeh amekataa kuachia madaraka ingawa muda wake ulipaswa kuisha jana. Bunge la nchi hiyo limemuongezea kipindi kingine cha miezi mitatu.
Rais huyo wa Gambia alipaswa kukabidhi madaraka kwa rais mteule, Adama Barrow anayepaswa kuapishwa muda wowote.
Jitihada za viongozi wa Afrika Magharibi kumshawishi Jammeh kukabidhi madaraka kwa amani zimegonga mwamba baada ya kusisitiza kuwa atabaki kuwa rais wa nchi hiyo akipinga matokeo ya uchaguzi ambayo aliyakubali awali.