Rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez, amefungua milango kwa Man City ili kufanikisha usajili wa Mlinda mlango kutoka nchini Costa Rica Keylor Navas.
Perez ametangaza kumuweka sokoni Navas itakapofika mwishoni mwa msimu huu, na ameona kuna umuhimu wa kufanya biashara na klabu ya Man City ambayo kwa sasa inahaha kusaka mlinda mlango akaekidhi hitaji la meneja Pep Guardiola.
Kiasi cha Euro milion 30 kimetajwa kama ada ya uhamisho wa mlinda mlango huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Costa Rica wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 pamoja na fainali za Copa America za mwaka 2015 na 2016.
Mpango wa kuuzwa kwa mlinda mlango huyo ambaye kwa sasa ndio changuo la kwanza la Real Madrid, umekuja kutokana na Perez kuanza kusaka namna ya kuwa na mlinda mlango mwingine ambaye atakuwa na vionjo vipya langoni mwa The Meringues.
Mlinda mlango wa sasa wa Man city Claudio Bravo ambaye aliaminiwa na Pep Guardiola wakati akisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, ameshindwa kutimiza wajibu wake kama alivyokua akifanya alipokua na FC Barcelona.
Usajili wa Bravo huko Etihad Stadium, ulisababisha kuondolewa kwa Joe Hart aliepelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Torino ya nchini Italia.