Sakata la utoaji ruzuku linalomkabiri Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Jaji Francis Mutungi, ameibuka na kusema kuwa hana hofu ya kuchafuliwa na kusema kuwa anamtambua Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu wake Maalim Seif kuwa ndiye Katibu Mkuu wa CUF.
Mutungi ameyasema hayo baada ya taarifa na kauli za kejeli zilizokuwa zikimhusu yeye na Ofisi yake kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii baada ya kuidhinisha zaidi ya Sh. milioni 300 za ruzuku kwenda kwenye akaunti ambayo kamati ya uongozi ya CUF imedai siyo ya chama hicho.
“Natambua uadilifu wangu na sitaki kuelezea, ila nahisi tukiendelea kuliongelea hili tutakuwa tunalikkuza bila sababu za msingi, Nasisistiza tena kuwa Ofisi yangu inamtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF, na Maalim Seif Hamad kama katibu Mkuu, si Mutungi aliyeiandika Katiba ya CUF ni wao wenyewe ndio walioiandika, Ofisi ya Msajili ilichokifanya ni tafsiri tu,”amesema Mutungi.
Aidha, taarifa za Msajili kuingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo na baadaye kutolewa kwa njia iliyokuwa inatia mashaka ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni huku akilinganisha suala hilo na uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.