Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeambiwa kuwa Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi utafungwa ifikapo Desemba mwaka huu, Kamati ilipata taarifa hiyo mara baada ya kufanya ziara na kuutaka Uongozi wa Mgodi huo uliopo Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga kufuata taratibu za ulipaji kodi.
Aidha, Meneja wa Mgodi huo Asa Mwaipopo, amesema kuwa ni kweli taarifa za kufungwa kawa mgodi huo zipo, lakini kwa hatua ya kwanza amesema ni kusitisha uchimbaji mwezi Desemba lakini shughuli zingine zitaendelea kama kawaida.
Amesema Mgodi huo kwa sasa una mawe kwaajili ya usagishaji ambayo yatachukua zaidi miaka miwili hivyo si rahisi kufungwa kwa siku moja,
Mwaipopo ameongeza kuwa wafanyakazi hawawezi kuachishwa moja kwa moja lakini watakuwa wanabadilishiwa shughuli za kufanya kulingana na ujuzi wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dotto Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Geita amesema kuwa katika Kampuni zinazowekeza nchini kwenye uchimbaji Madini baadhi zinakwepa kodi na kutishia kusitisha uchimbaji madini zinapodaiwa.