Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe, ametoa ufafanuzi kuhusu Rais John Magufuli kuteua Wabunge Wawili, pamoja na Naibu Waziri kuteuliwa kuwa Balozi, amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijakiukwa.
Ameyasema hayo mapema hii leo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo kimoja cha Redio, Mwakyembe amesema kuwa ameshangazwa na baadhi ya watu kushutumu teuzi hizo za Wabunge alizofanya Rais Magufuli, huku akisema Katiba ya Nchi inampa nafasi ya kuteua na kutengua nafasi ya mtu yeyote aliyemteua.
Aidha, Mwakyembe amesema kuwa ni vema watanzania wakamuacha Rais afanye kazi zake ikiwemo kufanya uteuzi mbalimbali kwa kuwa yeye ndiye anaona mtu gani anafaa wapi na nani amteue kwa wakati gani.
Jana , Rais John Magufuli, alifanya uteuzi wa mabalozi watano ambao ni pamoja na Dkt.Abdallah Possi ambaye kituo chake cha kazi na tarehe ya kuapishwa itatangazwa baadae,
Hata hivyo, Kabla ya kuteuliwa kuwa balozi Dkt. Abdallah Possi alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu aliyekuwa akishughulikia Walemavu.