Serikali imejipanga kupitia upya kanuni za utangazaji za Sheria ya Utangazaji ya mwaka 2003 ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye wakati wa ziara yake kwa vyombo vya habari vya Channel, na Tumain Media iliyolenga kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Serikali na vyombo vya habari nchini.
Nape amesema kuwa lengo la mapitio ya kanuni hizo ni uboreshwaji wa kanuni hizo ili kuisaidia kukuza sekta ya utangazaji.
“Kuna baadhi ya wadau wamekuwa wakilalamika kuhusu kupitwa kwa wakati kwa kanuni hizo, hivyo tumeona ni vyema kuungana nao ili kuzipitia upya na kuona palipo na mapungufu” amesema Nape.
Aidha, Nape ameongeza kuwa baadhi ya maeneo katika kanuni hizo yanayohitaji kupitiwa upya ni aina za leseni zilizopo, kubadilika kwa jamii inayotuzunguka pamoja na mabadiliko ya teknolojia yanayokuwa kwa kasi.
Mbali na hayo Nape amesema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ipo katika hatua za mwisho za kuandaa kanuni za kudhibiti masuala ya matumizi ya mitandao ya kijamii nchini.
Katika hatua hiyo Waziri Nape amewataka wadau mbalimbali kutoa maoni ili kusaidia kuboresha kanuni za mitandao ya kijamii kwa lengo ili kukuza tasnia ya habari.