Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Al-Haji Ali Hassan Mwinyi amewataka watanzania kuwa na tabia ya kuyafanyia muendelezo yale mema wanayoyafanya, kama walivyofanya kampuni ya NIDA TEXTTILE MILLS kusherekea kumbukumbu ya mazazi ya kiongozi wa waislamu Mtume Muhammad (S.A.W).
Akiwa katika hafla hiyo ya Maulid iliyofanyika lro Januari 22, 2017 jijini Dar es Salaam Al-Haji Mwinji ameeleza kuwa Mtume Muhammad alikuwa akifunga kila siku ya Jumatatu ikiwa ni ishara ya kusherekea siku aliyozaliwa hivyo ni vyema kuiga mfano huo wa kufanya matendo mema kwa kuyarudia mara kwa mara na kuyadumisha, huku akipongeza uongozi wa NIDA kwa kuwaalika na kusherekea pamoja kwani amejifunza mengi kupitia mawaidha yaliyotolewa na viongozi wa dini waliohutubia akiwemo Sheikh Ally Basaleh.
Sherehe hizo zimepambwa kwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Dini na Serikali akiwemo Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Gharib Bilal, Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Suleiman Jafo, Naibu Waziri Wizara ya Afya Hamis Kigwangala, Waziri wa zamani wa Ulinzi Profesa Juma Kapuya, Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba, Mbunge wa Mkuranga Juma Ulega huku kwa viongozi wa dini walikuwepo Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum na Kadhi Mkuu wa Tanzania Abdallah Mnyaa ambapo wote kwa pamoja walipewa zawadi maalum na kampuni hiyo.