Baada ya kimya kirefu cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha amesema kuwa uamuzi wake aliouchukua wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Urais wa Zanzibar wa mwaka 2015 baada ya kubainika kuwa na dosari, ulifanyika kwa kufuata taratibu, kanuni, Sheria na Katiba ya Zanzibar.
Jecha ameyasema hayo wakati akihojiwa na Kituo kimoja cha Televisheni na kusisitiza kuwa, hana wasiwasi wala hofu yoyote kwa hatua hiyo, aliyoichukua ya kufuta uchaguzi kwa kuwa ilifuata misingi yote ya Sheria na Katiba.
Amesema kuwa matatizo na dosari za uchaguzi huo, yalianza kujitokea katika kipindi cha kupokea matokeo ambapo matokeo yalitoka katika maeneo ya Unguja, hayakubainika kuwa na matatizo, isipokuwa kwa matokeo yalitoka katika maeneo ya Pemba.
“Tulikaa kimya kwa takribani mwezi mmoja tukisubiri hatua zichukuliwe na viongozi kupitia hivyo vikao vyao. Tulisubiri katika ule muda bila kuvunja sheria, na baada ya kuona hakuna hatua zinachokuliwa dhidi ya maamuzi yetu tulitangaza tarehe ya uchaguzi,” amesema Jecha.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo amekanusha madai kuwa ametumika kufuta uchaguzi huo kwa maslahi ya CCM na Dkt. Shein, na kuongeza kuwa hajawahi kukutana na mtu yeyote anayemlaumu kuhusu uamuzi wa tume hiyo wa kufuta uchaguzi,na endapo kuna mtu bado ana malalamiko, anaruhusiwa kuiandikia ZEC malalamiko yake na si yeye binafsi, yatafanyiwa kazi.