Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amefungua mafunzo ya siku tatu Mjini Dodoma ya wanasheria kutoka Halmashauri zote nchini huku akioneshwa kukerwa na tabia ya wanasheria hao kushindwa kesi na kuisababishia Serikali hasara kwa kuwalipa fidia washindi.
Jafo amesema zipo kesi nyingi zinazohusu halmashauri mbalimbali nchini zinashindwa kutetewa na kusababisha serikali kulipa fidia.
Amesema kuwa pamoja na kuwepo wanasheria ndani ya halmashauri hizo, lakini wanashindwa kusimamia kesi zinazowakabili hali inayochangia serikali kulipa gharama kubwa kwa washindi wakati fedha hizo zingetumika kwa maendeleo ya wananchi.
“Fedha zinazolipwa na serikali mara baada ya kushindwa kesi, zingeweza kusaidia maendeleo ya wananchi ndani ya halmashauri hizi kutokana na wanasheria kutokuwa makini,”amesema Jafo.
Amewataka kuhakikisha wanasimamia vyema kesi za ardhi zinazowakabili wananchi wa chini ambao wengi wao hudhurumiwa na wenye uwezo na kusababisha malalamiko kwa wasimamizi wa sheria.
Hata hivyo, amesema kuwa kutokana na sheria hizo kutoeleweka, inasababisha mikataba mingi ndani ya halmashauri hizo kutokuwa na umakini kwa kutoipendelea Serikali na kuwapa kipaumbele walioingia mikataba hiyo, hali inayoonyesha kama hawapo wanasheria.