Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli,amewaweka roho juu mawaziri wawili baada ya kuwapa siku moja kumpelekea haraka taarifa za makusanyo ya Fedha za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es salaam (BRT) tangu ulipoanzishwa.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli amewataka mawaziri hao kumpelekea taarifa kama mradi huo umeleta hasara au faida tangu kuanza kufanya kazi na kwamba hataki kusikia kitu kinachoitwa hasara.
Waliopewa maagizo hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.
“Ifikapo leo jioni,hawa mawaziri wawili na viongozi wa Dart wanieleze mradi huu umetengeneza faida kiasi gani, lazima wananchi wajue fedha zao zinakwenda Serikalini au mifukoni mwa watu,”amesema rais Magufuli.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizindua awamu ya kwanza ya huduma za BRT pamoja na miundombinu ya mradi wa mabasi ya Mwendo kasi Jijini Dar es salaam (DART) uliogharimu sh.bilioni 403.5.
Hata hivyo amesema kuwa mawaziri hao wametoa taarifa nzuri wakati wa uzinduzi huo,lakini wamewanyima raha kitu kimoja ambacho ni kiasi cha makusanyo ambacho kilichopatikana tangu kuanza kwa mradi huo.