Wananchi wametakiwa kuongeza juhudi katika kilimo kwani Serikali imejipanga katika kuhakikisha inaongeza thamani ya mazao yake kabla ya kuyauza nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Januari 25, 2017 wakati akizungumza na wakulima wa chai katika kijiji cha Lwangu wilayani Njombe ambapo ameeleza kuwa Serikali ilikuwa inapata hasara kwa kusafirisha malighafi nje nchi lakini kwa sasa inajenga viwanda ili iweze kuuza bidhaa.
“Miaka mingi Serikali imekuwa ikipata hasara kwa kuuza mazao nje ya nchi, tumeamua kujenga viwanda vitakavyoweza kuyachakata na kuuza bidhaa badala ya malighafi,”.
Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa viwanda ni moja kati ya mikakati ya dhati ya Serikali kuhakikisha mazao yanayolimwa ndani ya nchi yanakuwa na thamani kubwa hivyo kuongezea tija.
Amesema mazao hayo ndiyo yatakayoweza kuleta tija kwa wakulima, hivyo aliwashauri waendelee kushirikiana katika vikundi ili wapate misaada ya kitaalam kwa urahisi.
Aidha, Majaliwa amemuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Ruth Msafiri na Maafisa kilimo kuwatembelea wakulima hao kwa lengo la kuwaelekeza namna bora ya kuendeleza mazao yao.
Asema hatua hiyo itawawezesha wakulima kupata mbinu bora za kilimo na hatimaye kuvuna mazao mengi yenye viwango vya ubora vinavyotakiwa kimataifa.