Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka kuwachukulia hatua watumishi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa waliohusika na upotevu wa fedha za maendeleo zaidi ya sh. milioni 700 zilizopelekwa katika halmashauri hiyo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo sh. milioni 300 za ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri hiyo.
Majaliwa ametoa kauli hiyo Januari 26, 2017 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri alipokuwa katika ziara yake katika Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
“Mkuu wa Mkoa watu wote waliohusika na upotevu huu watafutwe popote walipo na kuchukuliwa hatua na kisha nipewe taarifa ya hatua ulizochukua. Hatuwezi kuwavumilia watu hao ambao wanachora ramani kwa sh milioni 200 na sh. milioni 100 zingine hazijulkikani zilipo,“ – Majaliwa.
Aidha, Majaliwa amemuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kufuatilia kiasi kingine cha sh milioni 400 zilizopelekwa wilayani hapo kwa ajili ya maendeleo ambazo nazo hazijulikani zilipo.
“Tafuta waliohusika popote walipo hata kama ni nje ya Njombe waje kutueleza ziliko fedha zetu,” amesema
Majaliwa pia ameuagiza uongozi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) kuhakikisha inashirikiana nayo inafanya uchunguzi ili kubaini watu waliohusika na upotevu huo.
Mbali na hayo, Majaliwa asema Serikali haitowavumilia watumishi wote wanaojihusisha na vitendo vya ubadhilifu wa fedha za umma, hivyo amewataka watumishi wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na maadili.
Amewataka watumishi wa umma nchini kuacha tabia ya kudokoa fedha za maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri zao kwa sababu Serikali iko macho na itawashughulikia wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Pia, Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wametakiwa kusimamia vizuri fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye maeneo yao na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Kabla, Waziri Mkuu alipokuwa njiani kuelekea Ludewa Mjini akitokea katika kata ya Mundindi Waziri Mkuu alisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Mlangali ambao waliiomba Serikali iwasaidie kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya maji.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Michael Lameck alisema alimueleza Waziri Mkuu kwamba awali walikuwa wanapata maji ila kwa sasa hayatoki kutokana na uchakavu wa miundombinu hali iliyowafanya kuchangishana na kupata sh. milioni 95 kati ya 200 zinazohitajika.
Mara baada ya maelezo hayo, Majaliwa amemuagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Nasib Mlenge kwenda kijijini hapo leo Januari 27 kukutana na Bw. Lameck ili kushirikiana naye na kuangalia alipofikia na kuendeleza uboreshaji wa miundombinu hiyo ili wananchi hao wapate maji.
“Mwenyekiti amechangisha sh. milioni 95 na kununua baadhi ya vifaa nyinyi mnashindwa nini. Lazima muwe makini na matatizo ya wananchi na Serikali haitaki masuala ya urasimu. Watu wana shida ya maji na mnajua tatizo mmekaa tu,” alisema.