Mshambuliaji M’Baye Niang amesajiliwa kwa mkopo na klabu ya Watford ya England akitokea kwa magwiji wa soka mjini Milan nchini Italia AC Milan.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, amelazimika kuondoka AC Milan kwa mkopo, kufuatia hali kuwa tete kwa upande wake, hasa linapokua suala la kucheza katika kikosi cha kwanza.
Meneja wa klabu ya Watford Walter Mazzarri, anaamini usajili wa Niang utasaidia kuondoa tatizo la upachikaji wa mabao kikosini mwake.
Klabu ya Watford inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka nchini England, na usajili wa mshambuliaji huyo kutoka nchini Ufaransa, unaaminiwa huenda ukaleta tija katika harakati za kuzisaka nafasi za juu kwenye msimamo huo.
Hata hivyo kuna uwezekano wa Niang kuendelea kubaki Vicarage Road, endapo ataushawishi uongozi wa klabu ya Watford ambao tayari umeshafikia makubaliano na AC Milan ya kufanya biashara ya kumsajili jumla itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Niang anakua mchezaji wa tatu kusajiliwa na Watford katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, akitanguliwa na mshambuliaji kutoka nchini Argentina Mauro Zarate akitokea Fiorentina pamoja na kiungo Tom Cleverley akitokea Everton.
Niang,alijiunga na klabu ya AC Milan mwaka 2012 akitokea nchini kwao Ufaransa kwenye klabu ya Caen inayoshiriki ligi daraja la kwanza (Ligue 1), na mpaka anaondoka San Siro alikua ameshafunga mabao 12 katika michezo 77 aliyocheza.
Aliwahi kutolewa kwa mkopo katika klabu za Montpellier (Ufaransa) mwaka 2014 na Genoa (Italia) mwaka 2015.