Simu yako ni sehemu ya sababu za kugombana mara kadhaa na mpenzi wako? Kama ndio, hauna tofauti na mastaa unaowakubali, Juma Jux na Vanessa Mdee.
Wasanii hao ambao licha ya kuwa ‘couple’ inayovuta umakini wa mashabiki wengi wa muziki kwa jinsi wanavyoonekana kuwa na furaha kama ndege Tetele, wamekiri kuwa kifaa hicho huwa sehemu ya mgogoro kati yao.
Vee money amefunguka kuwa yeye ndiye muathirika wa matumizi ya simu ya Jux ambaye mara kadhaa hujikuta hayuko hewani wakati mrembo huyo anabofya kitufe cha kijani cha simu yake akilisoma jina la ‘my hubby’ ‘my Juma’.
“Huwa tunagombana, sababu mara nyingi ni simu yake. Kuna wakati unakuwa unamtafuta hapatikani…,” Veemoney aliiambia Ngazi Kwa Ngazi.
Hata hivyo, uliibuka utani mzuri baada ya Jux kutaka kujitetea kuwa huwa anajikuta hapatikani kwasababu simu yake ya kupapasa huishiwa chaji.
Lakini mrembo wake akishindilia msumari kuwa chaji huwa sio sababu… “wakati nakuona Instagram!?” Hata hivyo, wawili hao wanajua jinsi ya kuirudisha furaha yao kwenye kilele.
Jux na Vanessa wanafanya vizuri na wimbo wao ‘Juu’.