Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka kesho ameagizwa kuwapeleka wakaguzi wa hesabu kwenda kukagua mapato na matumizi ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Njombe (NJUWASA) pamoja na kuangalia kama wananchi walihusishwa katika ukokotoaji wa gharama za malipo ya bili za maji.
Ole Sendeka amepewa agizo hilo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Mpechi, Halmashauri ya Mji wa Njombe
Agizo hilo la Majaliwa ni hilo baada ya wananchi kuilalamikia mamlaka hiyo kupitia mabango kwamba wanatozwa bili kubwa ya maji licha ya huduma hiyo kupatikana kwa kusuasua katika mji huo.
Kufuatia malalamiko ya wananchi, Majaliwa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa NJUWASA, Daudi Majani kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo ambapo alisema kwa mwezi wanakusanya sh. milioni 75 zinazotumika kuendeshea na uboreshaji wa huduma.
“Maji hakuna unasema unaboresha unaboresha huduma gani? Wananchi wanalalamika maji hakuna na mnawatoza gharama kubwa, Mkuu wa Mkoa kesho peleka wakaguzi wakakague kwa mwezi anakusanya kiasi gani na anafanyia nini,”